Riwaya: UCHU

PamojaForums · Sep 6, 2026 at 1:26 AMReplies 0 · Views 0
#1
UCHU

By A. E Musiba


SURA YA KWANZA


ARUSHA


Christopher Temu, ambaye Jumapili hii

Nyumbani kwake Arusha, alikuwa amefikiwa na

Ugeni mkubwa kutoka Umoja wa wanaharakati

Wa Afrika (Pan African Movement PAM) kutoka

Sehemu mbalimbali za Afrika. Temu alikuwa

Mwanachama wa chama hicho.

Hii haikuwa mara ya kwanza kwa watu hawa

Kukutana nyumbani kwa Temu kwani watatu

Kati yao walikaa nyumbani kwake kwa muda

Usiopungua miezi sita. Mnamo mwaka 1992 na

1993 walihudhuria mkutano uliofanyika Arusha

Kuvisuruhisha vikundi mbalimbali vilivyokuwa

Vikipambana katika mgogoro wa nchi ya

Rwanda, ili mgogoro huo umalizike kwa njia ya

Amani

Kikundi hiki cha PAM. Ambacho kilikuwa

Kinahudhuria kama kikundi cha wapenda amani

Wa Afrika. Kilikuwa kinaweka shinikizo kwa kila

Upande uliokuwa unahusika na mgogoro huo ili

Umalizike kwa amani. PAM ilianzishwa

Mwanzoni mwa karne ya 19 ikiwa na lengo la

Kupambana na utumwa, ukoloni mkongwe,

Ukoloni mamboleo, kupigania haki ya watu weusi

Na kuhakikisha kuwa waafrika wanaweza

Kupambanua mambo yao wenyewe.

Hivyo, mara hii kikao kilichokuwa kinafanyika

Nyumbani kwa Temu kilikuwa cha kutathmini

Juhudi zote zilizofanywa kuumaliza mgogoro wa

Rwanda kwa amani, lakini bila mafanikio.

Wakiwa wamekaa kwenye bustani nzuri

Iliyokuwa nyuma ya nyumba hii iliyojengwa

Kisasa. Ikiwa kwenye barabara ya Njiro kwenye

Kilima kidogo ikiuangalia mji wa Arusha kwa

Upande wa Kijenge. Mkutano uliendelea mchana

Huu wa saa kumi alasiri huku bia aina ya safari

Na ndafu, iliyokuwa inachomwa hapohapo

Kwenye jiko la mkaa vikiendelea kuwa

Viburudisho vya wageni hawa.

"Ndugu zangu. Fundisho kwa Rwanda ni

Fundisho kwetu sote, na sisi tukiwa tumejitolea

Kuona Afrika inajikomboa na kujitawala kwa

Amani ni lazima tukae chini kulitafakari swala

Zima la Rwanda tuone makosa yalitokea wapi,

Na kwanini hali ilifikia hapo ilipofikia na watu

Zaidi ya milioni moja kuteketea bila Afrika wala

Dunia kufanya chochote", Jackson Musoke

Kutoka Uganda ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa

PAM Kanda ya Afrika Mashariki alieleza.

"Ni kweli kabisa maneno uliyosema, lakini mimi

Nafikiri wakati mkutano wa amani ulipokuwa

Unaendelea hapa Arusha. Ukweli wa mambo

Rwanda ulikuwa haufahamiki. Na hivyo

Maamuzi mengi yaliyofanyika hayakuzingatia

Hali halisi ya mambo ilivyokuwa Rwanda wakati

Huo. Na ningependa niseme kuwa hata hivi sasa

Tunavyokaa hapa hali halisi na ukweli wa

Mambo Rwanda bado haujulikani. Ndiyo maana

Jumuia ya Kimataifa, Umoja wa Mataifa, Umoja

Wa Nchi Huru za Afrika bado wanafanya

Maamuzi ambayo yanazidi kuleta matatizo

Nchini humo, na kuifanya serikali ya sasa

Iyumbe katika kutekeleza shughuri zake za

Kuleta amani iliyo ya kweli katika nchi hiyo",

Alfred Kimani kutoka Kenya aliongezea.

"Sasa tutafanya nini ili huo ukweli wa mambo

Uweze kujulikana na matatizo yaliyo mengi

Katika nchi hiyo yaweze kutatuliwa?", Temu

Aliuliza.

"Mimi nafikiri tuunde tume ya uchunguzi,

Ikafanye uchunguzi, ichimbe chanzo cha

Matatizo Rwanda toka kabla ya uhuru mpaka

Sasa, na kujaribu kuelewa kabisa tatizo ni nini

Na nani anahusika na matatzo kwani mimi

Siamini kuwa tatizo hasa ni kabila tu. Miaka

Yote tumefikiria hivyo na kujaribu kumaliza

Tofauti za kikabila lakini mambo bado yako pale

Pale", Abdul Abakutsi toka Nigeria alijibu.

"Vilevile, kama tatizo ni la kikabila, lazima

Uchunguzi ufanyike ili ipatikane namna ya

Kulitatua tatizo hilo maana hatuwezi kukaa tu na

Kusema kwa sababu ni tatizo la kikabila, basi

Halina ufumbuzi", Lukaka Makwega kutoka

Zambia aliongeza.

"Tulipokuwa hapa kwa ajili ya mkutano wa

Amani, ilionekana kwamba serikali tawala ndiyo

Iliyokuwa inachochea ukabila. Swali hapa ni

Kwanini serikali inachochea ukabila?. Ni kwa

Sababu inataka kubaki madarakani kwa njia ya

Gawa utawale au Rais alikuwa na sera za

Kikabila yeye mwenyewe au kulikuwa na kitu

Kingine kilichokuwa kinachochea hali hii, maana

Kinachotisha zaidi ni jinsi mauaji hayo

Yalivyotokea. Inaonekana kuwa dakika ishirini tu

Baada ya ndege ilikuwa imemchukua Rais

Kutunguliwa mauaji yalianza sehemu zote. Hii

Inaonyesha mauaji yamepangwa kabla. Ina

Maana ilijulikana kuwa Rais atauawa siku hiyo?.

Na kama Rais ndiye aliyepanga mauaji haya, je

Alijuwa kuwa atauawa, na kwa hiyo akapanga

Akiuawa alipiziwe kisasi?. Na kama alijuwa

Atauawa kwani alirudi na ile ndege! Mimi vilevile

Naanza kukubaliana na wenzangu kuwa huenda

Kuna mambo zaidi yasiyojulikana ambayo

Yanaleta matatizo nchini humo. Nami naamini

Kuwa mambo hayo yakifichuliwa ufumbuzi wa

Matatizo ya ndugu zetu hao utapatikana

Haraka", Charles Malisa wa Tanzania alichangia.

"Kuna kitu kingine nilichokisema mwanzoni

Ambacho kinatisha sana. Jumuia ya Kimataifa

Haikufanya kitu chochote pamoja na kuona jinsi

Watu walivyokuwa wakiuawa kinyama. Majeshi

Ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa

Yalikuwepo. Na Jeshi la Ufaransa lilikuwemo

Nchini humo wakati wa mauaji. Nchi kama

Marekani ambazo zimejitokeza kama Polisi wa

Dunia, vilevile haikushtuka. Na kila mtu

Anakubali kuwa haya yalikuwa mauaji ya kikatili

Yaliyopangwa kuliko yale ya Hitler aliyowaua

Wayahudi. Kwanini hali ilibaki hivi! Na nchi za

Kiafrika nazo zilikaa tu zikiangalia kabila moja

Ndani ya nchi ya kiafrika likiangamizwa kabisa

Ili lisiwepo tena. Jamani hapa kuna sababu na

Kuna jambo ambalo halieleweki. Uchunguzi ni

Kitu cha lazima", Musoke alisisitiza.

"Abakutsi ametoa ushauri wa kuunda tume ya

Uchunguzi, sijui ni tume ya watu wa namna gani

Anayozungumzia, maana nchi yenyewe ya

Rwanda bado iko katika hali ya kivita bado

Wanauana. Serikali ya sasa bado haina uwezo

Wa kudhibiti hali ya usalama katika nchi hiyo.

Mambo yote bado shagalabagala. Tukisema

Watu kama sisi twende huko kufanya uchunguzi

Hakika hatutaambulia kitu kama si kutafuta

Kuuawa. Uchunguzi ni muhimu lakini lazima

Tufikirie uchunguzi huu ufanywe namna gani",

Makwega alishauri.

Watu wote waliohudhuria kikao hiki

Walinyamaza kimya wakitafakari kwa kina

Kuhusu uzito wa suala hili nyeti.

"Lete ndafu na utuongeze vinywaji, tunatakari

Huku tukilegeza makoo", Temu alimwagiza

Mtumishi wake. Bia baridi aina ya Safari

Zikaletwa na mabwana hawa wakaendelea

Kulegeza makoo na kutafuna ndafu, huku wote

Wakitafakari mazungumzo yao kwa makini.

Baada ya kimya kirefu Abakotsi alivunja kimya

Hicho. "Huenda ikawa ni lazima tuunde kikosi

Cha siri cha upelelezi, kipeleleze kwa sirisiri

Halafu kituletee taarifa maana serikali zetu zinao

Vijana wanaoweza kufanya upelelezi kama huo

Na ukazaa matunda. Kama bwana Makwega

Alivyosema, tume ya kawaida haiwezi kuambulia

Kitu, kwani mambo ni magumu huko. Nia yetu ni

Kupata ufumbuzi na si kupeleka watu

Wakauawe. Mnasemaje jamani?".

"Hapo umenena, hiyo ndiyo njia pekee ya kuweza

Kuingia ndani na kupeleleza kiini cha matatizo

Hayo. Mimi nakuunga mkono ila tutaiomba

Serikali gani itupe msaada huo?. Nyinyi

Wenyewe mliona jinsi serikali zetu

Zilivyonyamaza na kuacha kana kwamba

Hazikujua kuwa mauaji yalikuwa yakifanyika

Rwanda", Makwega alinena.

"Wote tunakubaliana kuwa njia nzuri ya kupata

Kiini cha matatizo yaliyosababisha hali ya

Rwanda ikafikia pale ni kutuma kikosi cha

Upelelezi?", Musoke aliuliza.

"Ndiyo", wote walijibu kwa pamoja.

"Basi, tuahirishe mkutano kwa leo, tuonane hapa

Kesho mchana saa kama hizi ili niweze

Kuwasiliana na watu fulani fulani ambao naamini

Wanaweza kutusaidia bila kugongana na serikali

Zetu", Musoke alisema.

Nyuso za wajumbe, ambazo kwa muda mrefu

Zilikuwa zikionyesha wasiwasi, zilikunjuka na

Kuonyesha furaha. Ndipo wote walipokumbuka

Kuwa Musoke ndiye aliyekuwa Mkuu wa Idara ya

Upelelezi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kabla

Haijavunjika. Hivyo, alijuana na wakuu wa idara

Hizi katika Afrika Mashariki, na alisemekana hadi

Sasa alikuwa akiombwa ushauri wa kiupelelezi

Mara kwa mara.

Baada ya kumaliza vinywaji vyao, wote

Waliondoka kuelekea kwenye hoteli zao

Walikofikia. Usiku ule Musoke aliporudi hotelini

Kwake, pale Mount Meru, aliwapigia simu rafiki

Zake, yaani wakurugenzi wa upelelezi wa Kenya,

Uganda na Tanzania. Alizungumza nao

Kidiplomasia na kila mmoja alimuomba ushauri

Na kumweleza sababu za kufanya hivyo. La

Kusikitisha ni kwamba, kwa vile yeye alikuwa

Sasa anaongoza chombo ambacho si cha

Kiserikali, serikali zisingeweza kumsaidia mtu au

Kikundi cha watu, kwa vile ingeshindwa kujieleza

Iwapo mkasa wowote wa kiupelelezi ungetokea.

Hilo ndilo lililokuwa jibu la kila mkurugenzi wa

Upelelezi. Wote waliomba samahani kwa hilo

Kwani walimheshimu sana, lakini ilikuwa nje ya

Masharti yao ya kazi, hasa wakati huu ambapo

Siasa za nchi hizi ni kutoingilia mambo ya ndani

Ya nchi zingine!

Swala hili lilimkasilisha sana Musoke. Wakati

Wenzao katika PAM wanapigania Afrika iwe

Moja, wengine wanadai eti ni kuingilia mambo

Ya ndani ya nchi nyingine!

"Ole wetu Afrika", Musoke alijililia. Ni wakati

Alipokaribia kukata tamaa, baada ya kufikiri

Sana namna ya kuweza kufanya ndipo

Alipomkumbuka Mzee mmoja mstaafu. Alifikiri

Huyu angeweza kumtatulia shida yake kwani ni

Mzee aliyeisaidia sana Afrika, hasa wakati wa

Ukombozi wa nchi zilizo kusini mwa Afrika. Yeye

Alijuana na wapelelezi wengi na maamuzi yake

Yalikuwa ya pekee, na ndiye aliyekuwa kitovu

Cha ukombozi Kusini mwa Afrika. Mpaka leo

Wengi walimjua kwa jina la "Chifu" tu.


ITAENDELEA....


 
No reactions yetReply / React
Continue the discussion on PamojaForumsOpen full thread